Dear Mama Samia,
Pole na majukumu. Pole pia kwa kuzushiwa taarifa kuhusu afya yako. Nitaongelea baadaye kuhusu hili la uzushi kuhusu afya za viongozi wetu.
Dear Mama, kilichonisukuma kukuandikia waraka huu ni vitu vitatu hivi vya msingi.
Cha kwanza ni matarajio ambayo mimi binafsi nimekuwa nayo tangu uingie mdarakani Machi 19, 2021. Matarajio hayo yalichangiwa na ukweli kwamba ulishuhudia kipindi kigumu ambacho Tanzania yetu ilipitia kati ya mwaka 2015 hadi 2021.
Na sio matarajio tu bali ulipoingia tu madarakani uliweka bayana vipaumbele vyako ikiwa ni pamoja na umoja na mshikamano wa kitaifa, na kimsingi, kuachana na siasa za chuki na visasi. Na umefanya mengi katika kufanikisha vipaumbele hivyo japo safari bado ni ndefu.
Cha pili, wewe ni Mama. Na kwa baadhi yetu, Mama ni upendo. Kuna watu wengi tu ambao hadi muda huu hawapendezwi na wewe kuitwa “Mama” lakini kwa baadhi yetu, u-Mama wako una maana kubwa sana, kwa sababu “penye Mama sio tu pana upendo, lakini pia hapaharibiki kitu.”
Cha tatu ni ukweli kwamba kufanikiwa kwako ni kufanikiwa kwetu sote. Naam, maraisi huja na kuondoka, lakini kwa wakati huu, Rais pekee tuliyenaye ni wewe. Na katika maisha yetu ya kila siku, kilichopo mkononi ni bora zaidi ya kinachotarajiwa ilhali hakipo mkononi. Hakuna binadamu mkamilifu, na hata kama kuna mapungufu ya kibinadamu katika uongozi wako, unabaki kuwa kiongozi bora tuliyenanye muda huu.
Ni kwa sababu hizo, na nyinginezo ambazo nafasi hairuhusu kuzitaja, baadhi yetu tunalazimika kukushauri, huku matarajio yakiwa kwamba hutochukulia ushauri huu kama ni ukosefu wa nidhamu.
Na kulazimika kutoa ushauri huu kunachangiwa pia na ukweli kwamba medani ya uongozi katika Tanzania yetu imetawaliwa na kasumba moja isiyopendeza, nayo ni unafiki.
Dear Mama, kuna wanafiki wenye jukumu la kukueleza ukweli/kukushauri, lakini hawafanyia hivyo kwa moja ya sababu hizi mbili. Aidha wanahofia wakikwambia ukweli wanaweza kuhatarisha ajira zao, au wanaacha kukwambia ukweli ili uharibikiwe. Hawa wa kundi la pili ni watu ambao hawakupaswa kuwa karibu nawe.
Lakini kuna tatizo pana zaidi, na hili ni la kitaasisi zaidi. Kuna taasisi zenye wajibu wa kukushauri. Nazo, aidha kwa mapungufu ya kiutendaji au kwa kuchelea “kuadhibiwa” endapo ushauri ukikataliwa, zinaishia kukwambia yake tu unayopenda kusikia.
Ukweli ambao tunaokupenda tunapaswa kukwambia
Paul Makonda anakufarakanisha na Watanzania wengi tu: Hadi muda huu watu wengi tu wanapata shida kuelewa vitu viwili. Cha kwanza ni uongozi wako kutochukua hatua stahili dhidi ya mtu huyu ambaye rekodi ya maovu yake huko nyuma ipo wazi. Cha pili, ni uamuzi wako wa kumzawadia uongozi licha ya rekodi hiyo ya huko nyuma.
Na hata ulipomteua Uenezi huko CCM na kufanya kila aina ya vituko, uliishia kumpongeza ulipomuondoa kwenye wadhifa huo. Huenda pongezi hizo zilikuwa lugha tu ya kisiasa, lakini picha iliyojengeka mtaani ni kwamba “kumbe vile vituko vya Makonda vilikuwa maagizo ya Mama?”
Kibaya zaidi ni kwamba huyu mtu amekataa katakata kujifunza kutoka kwenye makosa yake ya huko nyuma. Na yayumkinika kuamini kuwa kamwe hatojifunza. Moja ya sifa muhimu ya kiongozi ni unyenyekevu, sifa ambayo wewe Mama ni mfano hai katika hilo. Lakini huyo kijana wako amekuwa kinyume kabisa cha unyenyekevu ilionao Mama yetu. Ushahidi huu hapa
Mama yetu wewe sio tu ni mwanamke bali ni Mama yetu pia. Unajiskiaje kumuona kijana wako anafanya udhalilishaji dhidi ya mwanamke kiasi hiki?
Bahati nzuri Mwenyekiti wa UWT, Mheshimiwa Mary Chatanda, amekemea udhalilishaji huu
Kadhalika, shirika la haki za binadamu la LHRC nalo limekemea udhalilishaji huu
Ukiweka kando hili la udhalilishaji wa mtendaji huyo mwanamke, Makonda alikudanganya hadharani kuhusu “mawaziri wanaowalipa watu mtandaoni kukutukana wewe Mama yetu”.
Baadhi yetu tunapata shida kuona hadi leo, kiongozi huyo hajachukuliwa hatua kwa kukuongopea hadharani. Lakini kibaya zaidi, sio tu kwamba aliongopa, lakini ni mshirika na kada mmoja aliyedakwa akiwa na video na picha za viongozi mbalimbali na watu maarufu. Ni wazi kuwa Idara ya Usalama wa Taifa inafahamu kuhusu hilo, japo mtu huyo ambaye ni mtumishi wao, aliachiwa huru kwa “maagizo kutoka juu”.
Malalamiko mtaani
Dear Mama, pengine utashangaa “huyu nae anajuaje kuhusu malalamiko mtaani ilhali yeye kajificha huko nje ya nchi?” Ukweli ni kwamba uzalendo hauna makazi. Baadhi yetu tulio nje ya nchi – kwa sababu zozote zile _ tunaweza kuipenda Tanzania yetu zaidi ya wenzetu waliopo huko nyumbani. Hata hivyo simaanishi kuwa mie ni mzalendo zaidi ya mtu mwingine yeyote yule bali mapenzi kwa nchi yetu hutusukuma baadhi yetu kufuatilia mengi ya yanayojiri huko nyumbani.
Na ni katika kufuatilia huko, ndio nimeweza kufahamu malalamiko ya Watanzania wengi mtaani hususan kuhusu ugumu wa maisha ilhali viongozi mbalimbali wakiishi kama wapo peponi.
Watanzania wengi wanatambua umuhimu wa kuchagnia maendeleo ya taifa lao kwa njia ya kodi, tozo, nk lakini kuna hisia kuwa mchango wao kwa taifa lao unaishia kuwanufaisha mafisadi wanaotajwa kwenye orodha mfululizo za CAG pasi kuchukuliwa hatua zozote.
Hali hii inazua chuki kati ya wananchi dhidi ya serikali yao. Inajengeka taswira kuwa serikali haiwajali wananchi.
Kibaya zaidi, kuna wanafiki wengi wanazunguka huku na kule kukumwagia sifa – ambalo ni jambo zuri – lakini hawajibidiishi kukusaidia kwa kutekeleza vema majukumu yao katika sehemu zao za kazi.
Ni watendaji wachache tu wanaoweza kuonyesha kwa vitendo bidii/jitihada zao binafsi katika kuwatumikia wananchi na badala yake wanajificha katika kivuli cha “uchawa” kwako. Hakuna mwenye tatizo kwa wewe Mama yetu kusifiwa kwa kazi yako nzuri, lakini tatizo ni hao wanafiki ambao hawawatumikii wananchi ipasavyo lakini wako mstari wa mbele kukumwagia sifa kwa wananchi hao hao ambao matokeo yake baadhi wanapata hisia kuwa sifa hizo ni za uongo.
Hujuma kuelekea uchaguzi mkuu 2025
Dear Mama, japo pengine mimi si mtu sahihi kutanabaisha haya, lakini ukae ukifahamu kuwa unahujumiwa mno. Kuna jitihada za aina tatu hivi.
Kwanza, ni kukukwamisha usifike hiyo 2025. As to how, bila shaka watu wenye jukumu la kujua hilo wanajua, na kama hawajui, basi kuna tatizo kubwa, na kama wanajua lakini hawakwambii basi huenda nao ni miongoni mwa wanaotaka iwe hivyo.
Pili, ni kutengeneza mazingira magumu kwako kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kiasi kwamba uamue kwa hiari yako “kuwapisha wengine”. Kinachoongewa faraghani ni kwamba “yeye mwenyewe (yaani wewe Mama yetu) wala hakuwa na nia ya urais, ilimtokea tu”. Kuna jitihada za kujenga taswira kwamba hujali mammbo yakienda mrama kwa vile huenda ukawaachia wengine nafasi hiyo.
Tatu – na hili limekuwa endelevu – kukutengenezea mazingira kwamba bila watu flani, hutoweza kushinda urais mwaka 2025. Again, japo mie naweza kuwa sio mtu sahihi kutamka hili, naweza kutanabaisha bila shaka kuwa hakuna sababu moja ya msingi ya kukuzuwia kushinda urais katika uchaguzi mkuu ujao ON YOUR OWN.
Hitimisho
Dear Mama, katika zama hizi za “uchawa” ni rahisi kwa waraka huu kutafsiriwa kuwa ni jitihada za kujikomba, za kutaka kufikiriwa, na vitu kama hivyo. Uchawa unaathiri sana uzalendo, kwa sababu ni vigumu mno kwa sie wananchi wa kawaida kutenda jema kwa manufaa ya umma pasipo kujengeka hisia kuwa tuna ajenda binafsi.
Lakini kibaya zaidi, baadhi yetu hatutakiwi kuiongelea vema serikali na/au kukuongelea mema wewe binafsi. Kwa sababu tukiongea mema, inakinzana na narratives zao kuwa “huyu ni mhaini”. Na “wahaini” wanapaswa kuongelea mabaya tu.
Hata hivyo, la muhimu kwangu ni kutimiza wajibu wangu wa kiraia – na kitaaluma – kushauri pale inapobidi. Na njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kupitia jukwaa langu kama hili.
Uniwie radhi endapo chapisho hili litatafsiriwa kama kukukosea heshima. Nikutakie kila la heri katika utumishi wako kwa Tanzania yetu.
Kazi iendelee!